You are on page 1of 5

Kauli ya Serikali kuhusu matatizo katika Mtambo wa maji Ruvu Juu

1.Utangulizi
Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Mei, 2014 Mheshimiwa John Mnyika aliomba
Mwongozo wa Spika kuitaka Serikali itoe Kauli Bungeni chini ya Kanuni ya 49 ya
Kanuni za Bunge za Mwaka 2013 kueleza matatizo yanayoukabili Mtambo wa
kuzalisha na kutibu maji kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya DAWASA
katika Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, Mtambo wa Maji wa Ruvu Juu uliopo Mlandizi, wilaya ya
Kibaha ulijengwa mwaka 1954 1956 kwa ajili ya kuupatia maji Mji wa Da es
Salaam na maeneo yaliyopo kando ya Bomba kuu katika Wilaya ya Kibaha.
Uwezo wa mtambo huo kuzalisha maji ni lita milioni 82 kwa siku. Mtambo wa Ruvu
Juu unaendeshwa kwa kutumia seti tatu (3) za pampu katika shughuli za uzalishaji
maji.

Seti ya kwanza, yenye pampu nne, hutumika kuchota maji kutoka mtoni eneo la Ruvu
darajani mita 21 chini ya usawa wa ardhi kwa kiwango cha lita milioni 1.9 kwa saa;
kwa kila pampu.Pampu 2 hadi 3 hutumika kwa wakati mmoja kulingana na wingi na
kina cha maji kilichopo mtoni.

Seti ya pili; yenye pampu nnehusukuma maji ghafikutoka kwenye eneo la mto, kwa
kiwango cha lita milioni 1.4 kwa saa kwa mwinuko (head) wa mita 66 na umbali wa
kilomita 6 hadi Mlandizi kwenye mtambo wa kusafisha na kutibu maji.Pampu 3
hutumika kwa wakati mmoja kwa kazi hiyo.

Seti ya tatu ina pampu nne zinazosukuma majisafi kwenye mwinuko (head) wa mita
205 na umbali wa kilomita 65 kutoka Mlandizi hadi Kimara jijini Dar es Salaam.Kila
pampu ina uwezo wa kusukuma lita milioni 1.2 kwa saa.Ili kufikia uzalishaji halisi
pampu tatu hupaswa kutembea kwa wakati mmoja.

1.Hali ya Mtambo

Mheshimiwa Spika, mtambo wa Ruvu Juu kwa sasa umeshindwa kukidhi kiwango
cha maji kilichopangwa, yaani lita milioni 82 kwa siku kutokanana sababu zifuatazo:-

1.Kuharibika kwa pampumara kwa mara kunakosababishwa na uchakavu
unaosababishwa ba umri mkubwa (miaka 60);

2.Kukatika kwa umeme mara kwa mara;

3.Maji kuwa na tope jingi sana (turbidity) wakati wa mvua na mafuriko. Hii
hupunguza uwezo wa pampu za kusukuma maji na husababisha kusagika kwa vifaa
vya pampu;

4.Ugumu wa upatikanaji wa vipuri halisi (genuine parts) huchangia katika
kuchelewesha matengenezo.

2.Changamoto za Mtambo

Mheshimiwa Spika, kwa takribani siku 67 (kati ya tarehe 01.03.2014 na tarehe
06.05.2014) mtambo ulizalisha maji chini ya kiwango chake kutokana na matukio
yafuatayo:

1.Kuharibika kwa pampu 3 za maji ghafi raw water pumps (matukio 8);

2.Kuharibika kwa pampu za majisafi treated water pumps (matukio 2);

3.Kukatika kwa umeme(matukio 15,jumla ya saa 9 dakika 58);

4.Mafuriko katika bonde la mto Ruvu(siku 3; yaani kuanzia tarehe 12.04hadi
tarehe14.04.2014);

5.Kukatika kwa bomba la maji ya kupoza pampu za maji ghafi (katikaeneo la
mafuriko);

6.Kuungua kwa auto transformer kulikosababishwa na hitilafu ya umemekwa siku 2,
tarehe 25.04 hadi tarehe 26.04.2014;

7.Kiwango kikubwa cha tope katika maji ghafi (very high turbidity) ambacho
kiliongezeka kutoka 196 Nephelometric Turbidity Units (NTU) hadi 1,102 NTU.

3.Athari Zilizojitokeza

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto nilizokwisha eleza hapo awali,uzalishaji
maji ulipungua na kufikia kati ya lita milioni 8.2 nalita milioni 57.4ikilinganishwa na
lita milioni 82 kwa siku, ambazo ndio uwezo halisi wa mtambo huo. Uzalishaji
ulikuwa chini zaidi tarehe 18.04.2014 na kufikia lita milioni 1.9kutokana na mafuriko
na hitilafu kubwa ya umeme.

Kupungua kwa uzalishaji kuliathiri usambazaji maji na migao ya maji kwenye eneo
lote linalohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu. Maji kidogo yaliyozalishwa yaliishia
njiani kati ya Mlandizi na Kibaha, maeneo ya Tabata na Kimara yaliathirika zaidi.

4.Jitihada za Serikali katika Kukabiliana na Changamoto za Mradi
Mheshima Spika, Wizara katika kukabiliana na matukio hayo,imechukua hatua
zifuatazo:

1.Kuchonga vipuri na vifaa vya pampu katika karakana zilizopo hapa nchini kwa
kuwatumia wataalam wa Jeshi;

2.Kuagiza vipuri nje ya nchi; na

3.Kutoa matangazo kwa wananchi kuhusu upungufu wa maji pale uzalishaji
unapopungua/kusimama.

Mheshimiwa Spika, kwa nyakati tofauti matengenezo yamechukua muda mrefu
kidogo kutokana na kutopatikana kwa wakati mali ghafi zinazohitajika, mfano chuma
cha high carbon steel kwa ajili ya shaft za pampu na bearing housing cover. Vifaa
vilivyoagizwa nje ya nchi ni roller bearings pamoja na valvu za kuzuia maji kurudi
kwenye pampu (non-return valve) kwa ajili ya seti ya pampu za maji ghafi. Bearings
zote za akiba zilikwisha baada ya pampu namba 3 kuharibu bearings 2 na pampu
namba 4 kupasua bearing 1; pampu zote hizi ni za maji ghafi.

Mheshimiwa Spika, auto transformer nne ziliagizwa kutoka Switzerland zimewasili
na kufungwa kwenye kituo cha Mlandizi. Auto transformer hutumika kupoza umeme
kwa ajili ya pampu za maji safi. Bomba la pili la maji ya kupoza pampu limeongezwa
ili kuepuka utegemezi wa bomba moja tu lililopo kwenye eneo la tindiga la maji
lililopo kwenye mashamba ya JKT Ruvu; kati ya mto Ruvu na mji wa Mlandizi.Lengo
ni kuokoa muda wa kuzima pampu endapo bomba mojawapo la maji ya kupoza
pampu litapata hitilafu.

Mheshimiwa Spika, baada ya jitihada kubwa zilizotajwa awali, uzalishaji wa Maji wa
Mtambo wa Ruvu Juu unaendelea kurudi katika hali yake ya kawaida; kwa mfano
tarehe 17 Mei, 2014 uzalishaji wa maji ulifikia lita milioni 80.8 kwa siku, tarehe 18
Mei, 2014 uzalishaji ulikuwa lita milioni 80.3 kwa siku, lakini tarehe 19 Mei, 2014
uzalishaji ulishuka ukafikia lita milioni 70.8 kwa siku, kutokana na kukatika kwa
umeme kwa masaa matatu (3).

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchukua hatua za dharura, vifaa na vipuri vya ziada
viliagizwa kutoka nje ya nchi na vingine kuchongwa katika karakana za ndani na
kuvihifadhi kwa ajili ya dharura. Hivi sasa zipo seti 2 za pampu kwa ajili ya dharura.
Aidha, mtambo wa kuchotea maji mtoni unafanyiwa ukarabati sasa na kama sehemu
ya kazi hiyo, DAWASA wameagiza pampu mbili mpya kwa ajili ya kuchotea maji
ghafi katika intake; pampu hizi zitawasili mwezi Agosti, 2014. Mkandarasi
amekamilisha tathmini ya ukarabati unaohitajika ili mtambo ufanye kazi vizuri katika
kipindi chote cha mpito cha miezi 18 wakati mtambo mpya unajengwa.

Jitihada nyingine za Serikali

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na jitihada za kudhibiti uwizi mkubwa wa
maji unaofanyika katika Jiji la Dar es Salaam yakiwemo maeneo ya Kinondoni,
Mwananyamala, Kigogo, Mabibo, Magomeni, Tegeta, Kiluvya, Kibamba, Mbezi na
Kimara. Mwezi Aprili 2013, Serikali iliunda kamati ya kufuatilia tatizo hilo la wizi
wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani. Jumla ya watuhumiwa wa
wizi wa maji 162 walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Hadi sasa, watuhumiwa
23 walipatikana na hatia ambapo watuhumiwa 19 waliamuriwa kulipa faini kati ya
shilingi 200,000 hadi 2,316,400 na watuhumiwa wanne (4) walifungwa.

5.Mpango Uliopo Sasa

Mheshimiwa Spika, kwa kutumia mkopo kutoka Serikali ya India, Serikali
imemwajiri Mkandarasi Va Tech Wabag kutoka India kujenga upya na kupanua
mtambo wa Ruvu Juu. Upanuzi huu utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni
82 hadi lita milioni 196 kwa siku. Gharama ya Mradi huu ni Dola za Marekani milioni
39.7. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na; kukarabati miundombinu yote iliyopo sasa,
kujenga intake bay mpya, kujenga miundombinu ya kuondoa tope kabla ya kuchota,
kujenga kituo kipya cha pampu za maji ghafi, kujenga bomba jipya la maji ghafi,
kupanua na kuongeza machujio ya maji, kujenga matanki ya hifadhi, kukarabati na
kupanua mfumo wa umeme na kujenga kituo kipya cha pampu za maji safi.
Mkandarasi alianza kazi tarehe 15 Februari 2014 na ujenzi unatarajiwakukamilika
tarehe 14 Agosti 2015.

Aidha, Mkandarasi mwingine Megha Engineering Ltd, pia kutoka India, ameanza kazi
ya kulaza bomba jipya la kipenyo cha milimita 1,200 kutoka Mlandizi hadi Kibamba
ambapo atajenga tanki lenye ujazo wa lita milioni 10. Pia mkandarasi huyo atajenga
bomba la kipenyo cha milimita 1,000 kutoka tanki la Kibamba hadi katika matenki ya
Kimara. Mradi huu umeanza kutekelezwa tarehe 10 Machi, 2014 na unatarajiwa
kukamilika tarehe 9 Septemba, 2015 na utagharimu Dola za Marekani milioni 59.3.
Mheshimiwa Spika, kazi zote hizi zitakapo kamilika uhaba wa maji kwenye maeneo
ya Mlandizi, Kibaha, Kiluvya, Kibamba, Mbezi, Kimara, Ubungo na Tabata utaisha.

6. Hitimisho

Mheshimiwa Spika, Kumekuwa na matukio mengi na ya kufululiza ya kuathiri
uzalishaji wa maji katika mtambo wa kusafishia maji wa Ruvu Juu. Matatizo hayo
yamehusu kuharibika kwa pampu, umeme kukatika mara kwa mara na kupasuka kwa
mabomba. Wizara imeunda Kamati maalum ambayo imeanza kufanya tathmini ya
kina ili kujua chanzo cha matukio hayo ambayo yamekuwa yakifululiza.Kamati hiyo
itafanya uchunguzi kubaini kama matatizo hayo yanatokana na mifumo ya kiufundi,
kiuendeshaji au makosa ya kibinadamu. Kamati inatarajiwa kutoa taarifa yake katika
kipindi cha mwezi mmoja na hatua zitaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha mtambo
unarudi katika hali yake ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe na Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza.

PROF. JUMANNE A. MAGHEMBE (MB)
WAZIRI WA MAJI
Dodoma, Mei 2014.

You might also like