You are on page 1of 4

Ni katika Hotuba yake ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya Wizara ya

Habari,Utamaduni na Michezo aliyoiwasilisha Bungeni leo hii muda mfupi


uliopita. Waziri Kivuli Joseph Osmundi Mbilinyi aka Sugu amemtaja Zitto Z.
Kabwe kama Mmiliki wa Kampuni ya Leka Dutigite aliyofanya biashara isivyo
halali na Mashirika ya Umma ya NSSF na TANAPA.

Sehemu husika ya Hotuba hiyo ni hii:

Mheshimiwa Spika, Tarehe 13 Agosti, 2012, Msajili Msaidizi wa Makampuni
katika Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni (BRELA) alitoa Hati ya
Usajili (Certificate iof Incorporation) kwa kampuni inayoitwa Leka Dutigite
Limited. Kwa mujibu wa nyaraka za BRELA, Leka Dutigite Ltd. ina ofisi zake
katika ghorofa ya kwanza ya jengo la City House lililoko katika Mtaa wa
Mkwepu, Dar es SalaaM. Mheshimiwa Spika,

Katiba, yaani Memorandum and Articles of Association, ya kampuni ya Leka
Dutigite Ltd. iliyosajiliwa BRELA tarehe 13 Agosti, 2012 inaonyesha kwamba
mwenye hisa nyingi katika kampuni hiyo ni kampuni nyingine inayoitwa
Gombe Advisors Ltd. ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za kibenki ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge
lako tukufu imezipata, mnamo tarehe 10 Desemba, 2012, Hifadhi ya Taifa ya
Saadani ilihamisha jumla ya shilingi 12,200,000 kwenda kwenye akaunti na.
0150357447800 iliyoko CRDB Bank tawi la Pugu Road, Dar es Salaam,
inayomilikiwa na Leka Dutigite Ltd. Hifadhi ya Taifa ya Saadani inamilikiwa
na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), ambayo ni shirika la umma. Siku
moja baadae, fedha hizo zilitolewa kwa pesa taslimu kutoka kwenye akaunti
hiyo.

Baada ya hapo, kati ya tarehe 14 Januari na 7 Februari, 2013, akaunti ya Leka
Dutigite Ltd. iliingiziwa jumla ya shilingi 28,600,000. Fedha hizi zote
ziliingizwa kama fedha taslimu na mtu aitwaye Mchange (shilingi 3,600,000
tarehe 14 Januari, 2013) na Leka Dutigite (shilingi 25,000,000 tarehe 23
Januari na 7 Februari, 2013). Kufikia tarehe 7 Februari, 2013, fedha hizo zote
zilikwishatolewa benki.

Mheshimiwa Spika, Tarehe 28 Februari, 2013, akaunti ya Leka Dutigite Ltd.
iliingiziwa shilingi 32,367,000 na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF). Kwa mujibu wa taarifa za kibenki, siku hiyo hiyo, fedha hizo zilitolewa
kwenye akaunti hiyo. Siku nne baadae, yaani tarehe 4 Machi, 2013, NSSF
ilifanya malipo mengine kwenye akaunti ya Leka Dutigite Ltd., kwa mikupuo
miwili, ya jumla ya shilingi 46,663,000. Siku hiyo hiyo, fedha hizo nazo
zilitolewa kutoka kwenye akaunti hiyo kwa mikupuo miwili. Kwa hiyo, katika
kipindi cha miezi mitatu katika ya tarehe 10 Desemba, 2012 na 4 Machi, 2013,
Leka Dutigite Ltd. ililipwa shilingi 119,930,000 kwa utaratibu huo huo wa
ingiza na toa fasta. Kati ya fedha hizo, shilingi 12,200,000 zililipwa na
TANAPA na shilingi 79,027,000 zililipwa na NSSF.

Mheshimiwa Spika, Katika mazingira ya kawaida, sio kitu cha ajabu kwa
mashirika ya umma kama NSSF na TANAPA kufanya biashara na watu au
taasisi mbali mbali kama makampuni binafsi. Ukweli ni kwamba, kwa upande
wa malipo yaliyofanywa na TANAPA, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako
tukufu imeweza kupata nakala ya mkataba unaohusu Maandalizi ya Filamu
(Documentary) kwa Ajili ya Kuhamasisha Shughuli za Utalii katika Hifadhi ya
Taifa ya Saadani kwa Kutumia Wasanii Kutoka Kigoma. Mkataba huo
umesainiwa tarehe 5 Desemba, 2012, kati ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na
Leka Dutigite Ltd. na una thamani ya shilingi 12,200,000, kiasi kile kile
kilicholipwa na Hifadhi hiyo.

Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, mazingira ya malipo haya sio ya kawaida. Hii
ni kwa sababu ya uwepo wa kampuni ya Gombe Advisors Ltd. Kwa mujibu wa
nyaraka za BRELA, kampuni hii ilisajiliwa tarehe 24 Novemba, 2011. Kwa
mujibu wa nyaraka hizo, ofisi za Gombe Advisors Ltd. ziko kwenye jengo la
City House, Mtaa wa Mkwepu, Dar es Salaam, ziliko ofisi za Leka Dutigite Ltd.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, wakurugenzi wa Gombe Advisors Ltd. ni Zitto
Zuberi Kabwe ambaye kazi yake inatajwa kuwa mchumi, na Raphael Ongangi
ambaye anatajwa kuwa mchambuzi wa fedha na vitega uchumi (Financial
and Investment Analyst). Bwana Ongangi aliwahi kutajwa na gazeti la kila
wiki la ----- la tarehe 26 Desemba 2013 kuwa ni mmoja wa washauri wa Zitto
Zuberi Kabwe na anasemekana kuwa msaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, Zitto Zuberi Kabwe sio mchumi anayetajwa katika
nyaraka za BRELA zinazoihusu kampuni ya Gombe Advisors Ltd. pekee, bali
pia ni Mbunge, tangu mwaka 2005, wa Bunge lako tukufu. Kama Mbunge,
Mheshimiwa Zitto Kabwe ni kiongozi wa umma kwa mujibu Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, 1995. Sheria hii inawalazimu viongozi wa
umma, wanapokuwa madarakani, kuwa waadilifu, wenye huruma, utulivu,
umakini na watakaoendeleza viwango vya juu vya maadili ili kujenga na
kuendeleza imani ya umma kwa uadilifu wa Serikali.

Aidha, viongozi wa umma ... watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma
na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na
kuthibitika kuwa ni wazi kwa umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu
wao kwa kufuata sheria tu. Vile vile, kuhusiana na maslahi binafsi, Sheria hii
inaelekeza kwamba ... viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi
ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika
kuyafanya.

Mwisho, kuhusiana na maslahi ya umma, viongozi wa umma wanatakiwa, pale
wanapochaguliwa au kuteuliwa, kupanga masuala yao kwa namna
itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana
kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na
maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma. Kwa
kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu,
Mheshimiwa Zitto Kabwe hajawahi kutangaza maslahi aliyonayo kwenye
mikataba ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite Ltd. na NSSF na TANAPA.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe sio tu ni Mbunge
anayebanwa na masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, bali pia
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC).
Kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu
za Bunge lako tukufu, mojawapo ya majukumu ya PAC ni kushughulikia
maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika
Wizara na Mashirika ya Umma yaliyoainishwa katika taarifa ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. NSSF na TANAPA ni baadhi tu ya
Mashirika ya Umma yaliyo chini ya usimamizi wa kibunge wa PAC.

Kwa maana hiyo, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Zitto Kabwe, kwa kutumia
makampuni yake ya Leka Dutigite Ltd. na Gombe Advisors Ltd., amefanya
biashara na TANAPA, shirika la umma analolisimamia kama Mbunge na
Mwenyekiti wa PAC. Mheshimiwa Zitto Kabwe na wanamuziki washirika
wake, kwa kutumia makampuni ya Gombe Advisors Ltd. na Leka Dutigite
Ltd., wamelipwa fedha za umma za TANAPA na NSSF.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa maelezo juu ya madai ya
ukiukwaji wa Sheria uliofanywa na viongozi wa umma na mashirika ya umma
katika kashfa hii. Pamoja na maelezo yatayotolewa , Kambi Rasmi ya Upinzani
inataka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum
juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa na TANAPA na NSSF; msukumo
uliofanya fedha hizo zitolewe na matumizi ya fedha hizo kwa kuzingatia
masharti yanayosimamia fedha za umma na utawala bora katika usimamizi wa
fedha za umma. Aidha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) ifanye uchunguzi juu ya malipo na matumizi husika kwa
kurejea masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Sheria
nyingine zinazohusika. Kwa upande mwingine, kwa kuwa suala hili linahusu
mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge inayohusika na usimamizi wa
fedha za umma, Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge nayo ifanye
uchunguzi wake juu ya madai ya masharti ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge na Kanuni za Bunge juu ya maadili ya kiongozi
wa umma ikiwemo yahusuyo utangazaji wa maslahi.

Mheshimiwa Spika; Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu
inatoa rai kwa wanamuziki na wasanii wengine wote nchini kuwa waangalifu
na watu wanaotaka kutumia umaarufu wao kama wanamuziki na wasanii kwa
lengo la kufanikisha dili za kifisadi. Bila kuchukua tahadhari ya kutosha,
wasanii hao wanaweza kujikuta wakipoteza sifa na umaarufu wao ambao
wameujenga kwa jitihada zao wenyewe.

You might also like