You are on page 1of 6

Kashfa Saba zilizo ikumba Tanzania Kipindi Cha Kikwete.

Dar es Salaam. Serikali imepoteza zaidi ya Sh362.9 bilioni kutokana na baadhi


ya kashfa kubwa za ufisadi na operesheni mbalimbali zilizoligharimu taifa
tangu uhuru.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini taifa kukumbwa na kashfa mbalimbali za
upotevu wa fedha au kuanzisha mipango ambayo utekelezaji wake
ulisababisha maumivu kwa wananchi na hakuna awamu ya uongozi wa
Serikali iliyokwepa hali hiyo.

Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere aliyeiongoza nchi toka
mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi (1986-1995),
Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais Jakaya Kikwete (2005-hadi sasa),
kumeibuka kashfa mbalimbali, saba zikiwa kubwa na kulitikisa taifa.

Kashfa na operesheni saba kubwa zilizotikisa taifa ni pamoja na Operesheni
Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa
kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support CIS) na Kashfa ya Rada.

Nyingine ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya Richmond, Operesheni
Tokomeza Ujangili na ile ya uchotaji mabilioni katika akaunti ya Escrow.

Operesheni Uhujumu Uchumi

Mwaka 1984 Serikali ilianzisha Operesheni Uhujumu Uchumi, iliyoongozwa
na Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine ili kutaifisha mali ambazo
baadhi ya watu walidaiwa kujipatia kwa njia isiyo halali.

Operesheni hiyo ilishuhudia baadhi ya watuhumiwa wakimwaga fedha
mitaani na majalalani, huku wengine wakitupa mali kuhofia kutiwa kwenye
mkono wa sheria.

Hata hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya watendaji wa Serikali ambao
hawakuwa waaminifu, waliitumia nafasi hiyo vibaya kutaifisha mali za baadhi
ya watu, ambao hawakuwa wahujumu uchumi.

Zoezi hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa vijijini kuwekwa ndani na
wengine kuachwa maskini baada ya kunyanganywa mali zao ikiwamo mifugo
na mashine za kusaga nafaka, kwa kudaiwa kuwa walizipata kwa njia isiyo
halali.

Mfuko wa Commodity Import Support (CIS)

Miaka 24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka sakata jingine lililokuwa na
harufu kubwa ya ufisadi wa mabilioni katika Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji
Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support CIS).
Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara maarufu
nchini na wizara kadhaa za Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya
Zanzibar (SMZ).

Kupitia mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi ya Sh200 bilioni kwa kivuli cha
uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi.

Mfuko huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya 1980, ambapo baadhi ya nchi
wafadhili ikiwamo Japan, zililenga kuipatia Tanzania fedha za kigeni za
kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa barabara, vifaa vya kilimo, ujenzi
na vingine mbalimbali. Mpango huo ulioanzishwa na Serikali uliendelea hadi
mwanzoni mwa miaka 2000, ambapo nchi hizo wahisani ikiwamo Japan,
Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia, Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na
Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali fedha za kigeni ili kuimarisha sekta za
biashara.

Wizara zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa CIS ni pamoja na iliyokuwa ya
Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kazi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji
na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa Tanzania Bara, wakati Zanzibar zinatajwa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Maji.

Rada

Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine.
Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada
kuukuu kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo
unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa Sh29.5 bilioni, wakati
gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.

Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha hizo kama chenji, huku
ikisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa hapa nchini waliohusika na ununuzi wa
rada hiyo mtumba, washitakiwe Tanzania au Uingereza kutokana na
kubainika dosari kwenye ununuzi huo.

Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, mtandao
wa Wikileaks unaosifika kwa kufichua siri za ndani ya mataifa mbalimbali
duniani, ulibaini kuwepo kwa harakati nchini za kutowafikisha mahakamani
wahusika wa ufisadi huo.

EPA

Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa mabilioni katika Akaunti ya
Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu (BoT), ambapo vigogo
kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya Sh133 bilioni katika akaunti
hiyo.

Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa
katika kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki wa nyaraka hizo.

Richmond
Mwaka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kulitokea
tatizo kubwa la uhaba wa umeme.

Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja
na kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo.

Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alikuwa mstari wa mbele katika
mikakati hiyo ndipo Kampuni ya Richmond Development (LLC) ilipewa
zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura na kuliuzia Shirika la Ugavi wa
Umeme nchini Tanesco.

Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa
kuzalisha umeme kama ilivyodhaniwa, badala yake kulikuwa na michezo
michafu iliyofanyika kwa masilahi ya wafanyabiashara na baadhi ya viongozi
wa Serikali.

Mwaka 2007, sakata hilo lilifika bungeni na aliyekuwa Spika wakati huo,
Samuel Sitta aliunda kamati iliyokuwa chini ya mbunge wa Kyela, Dk
Harrison Mwakyembe ili kuchunguza suala hilo.

Kamati hiyo ilichunguza sakata hilo na kutoa taarifa ilionyesha kuhusika kwa
viongozi wa juu wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa
na kusababisha kiongozi huyo, kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili kungoka
madarakani.

Waliongoka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi
tofauti, ambao ni Naziri Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.

Operesheni Tokomeza Ujangili

Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na Serikali kupambana na
ujangili wa wanyama nchini mwaka jana iliwangoa madarakani mawaziri
wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa kusimamia vizuri utekelezaji
wa operesheni hiyo.

Kungoka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua uteuzi wao baada ya
kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini Marekani.

Mawaziri waliongolewa kutokana na ripoti ya kamati hiyo iliyoongezewa
shinikizo na michango ya wabunge wengi ni Waziri wa Maliasili na Utalii,
Khamisi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai
Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David
Mathayo.

Operesheni hiyo inadaiwa kukiuka haki za binadamu ikiwamo watu 13 na
askari sita kuuawa, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa, ubakaji, rushwa na
uporaji wa mali za wananchi.

Akaunti ya Esrow

Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika, mapema mwaka huu imeibuka
kashfa ya upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye Akaunti ya Esrow katika
Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kashfa hiyo inayolitikisa Bunge na Serikali sasa, imetajwa kuwa ni
mwendelezo wa jinamizi la kashfa ikiwa ya saba kubwa kulikumba taifa hadi
sasa.

Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni, ilifunguliwa wakati kukiwa
kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa zamani wa IPTL (VIP
Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya Malaysia) kwa
upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT, kwa upande
mwingine.

Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa kuchukua kitu chochote hadi pale
mgogoro utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita hicho cha fedha kilichotwa.

Wazungumza

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya
alisema matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana na Serikali
kushindwa kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu
wanapatikana na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.

Alisema kila mara wizi wa fedha za umma unapotokea, Serikali hupata
kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua inayowafanya watu wengi kuamini
kushindwa kwao kunatokana na woga wa kutekeleza azma zao.

Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani, kuna kulindana sana,
lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi pengine ufisadi usingekuwa
wa kiwango cha juu namna hii, alisema.

Mhadhiri

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) Faraji Christoms,
alishauri wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa wanatakiwa
kujitathmini upya.

Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa tathmini kuwa ni uzalendo kwa taifa,
elimu kwa maana ya uelewa wa mambo ya kisheria, lugha za kimataifa na
umakini wakati wa majadiliano ya kimataifa na wanaposoma mikataba ya aina
hiyo.
Unakuta mtu badala ya kutuliza akili akasoma kwa makini mkataba kabla ya
kuusaini, anaupeleka kwa msaidizi wake ukisindikizwa na memo (agizo la
maandishi) Please read carefully for advice, (tafadhali soma kwa makini,
shauri), alieleza Christoms.

Alisema katika mazingira hayo, hatima ya usalama wa mkataba huo unakuwa
mikononi mwa mwingine, tofauti na aliyepewa dhamana.

Christoms alisema mazingira yanaonyesha kuwa wanasheria serikalini
wanashindwa na walioajiriwa kwenye kampuni za uwakili, hivyo kusababisha
Serikali kupata hasara kwa kuingia katika mikataba isiyo na masilahi kwa
taifa.

Profesa Gaudence Mpangala, wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO) alisema
historia ya ufisadi nchini inamnyima mtu yeyote makini, ujasiri wa kuishauri
Serikali mbinu za kudhibiti vitendo hivyo vya rushwa.

Profesa Mpangala alisema vitendo vya rushwa haviepukiki katika jamii, lakini
Serikali inapochukua hatua zinazothibitisha kuwa inavipiga vita, hali inakuwa
shwari tofauti na ilivyo nchini ambapo rushwa ndogo na ufisadi vimeota
mizizi huku hatua zinazochukuliwa zikiacha maswali mengi bila majibu.

Alitoa mfano wa serikali ya awamu ya kwanza, ilivyoshughulikia rushwa
iliyokuwa inaelekea kwenye ufisadi kwa kuchukua hatua kali, chini ya hayati
Edward Sokoine na Mwalimu Nyerere ambapo waliothibitika kuhusika
pamoja na adhabu ya kifungo jela, walitakiwa kuchapwa viboko wakati wa
kuingia na kutoka

You might also like