You are on page 1of 4

TGNP MTANDAO

S.L.P 8921, Dar es Salaam, Tanzania; Barabara ya Mabibo


Simu; 255 22 2443450/ 2443205/ 2443286; Selula; 255 754 784050; Faksi; 255 22 443244;
Barua Pepe; info @tgnp.org; Tovuti; www.tgnp.org

BAJETI YA TAIFA 2015/16


JE BAJETI HII NI YA WANANCHI AU YA UCHAGUZI MKUU?
TGNP Mtandao kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya jamii kutoka maeneno mbali mbali ya Dar es
Salaam, Mbeya, Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS),
Kikundi Kazi cha Uchambuzi wa Bajeti (BATT) tunatoa tamko hili baada ya kufanya uchambuzi na
kuanisha maboresho na mapungufu ya bajeti ya taifa ya 2015/16 iliyosomwa na Waziri wa Fedha na
Uchumi Mh. Saada Salum Mkuya tarehe 11 Juni 2015 Bungeni Dodoma.
Kwanza tunaipongeza serikali kwa kuonesha nia madhubuti ya kukabiliana na upotevu mkubwa wa
mapato kwa kurekebisha sheria mbali mbali za kodi. Pia Tunapongeza kuondolewa kwa mamlaka ya
waziri wa fedha kutoa misamaha ya kodi, hii ni hatua nzuri ya kuweza kukabiliana na ufisadi, rushwa na
watu wachache kunufaika na misamaha ya kodi. Vile vile tunapongeza serikali kwa kuongeza pensheni
ya wazee kutoka 50,000/= mpaka 85,000/= yaani ongezeko la asilimia 70% . Kupunguza utegemezi wa
bajeti hadi kufikia 6.4%, kuongezwa kwa kodi ya bidhaa zitokazo nje ya nchi mfano sukari ili kulinda
soko la ndani; kuondolewa kwa kodi ya vifaa vya uvuvi pembejeo za kilimo, vifaa tiba na bidhaa za
mitaji; kuongezwa kwa kodi ngozi ghafi ili kulinda viwanda vya ndani na serikali kutofanya kazi na
wazabuni wasiolipa kodi. Serikali kubadilisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa
kielectronic, hii itasaidia udhibiti wa mapato toka ngazi ya serikali ya mtaa kama vile mahakamani,
shuleni, hospital, trafic nk; uwekezaji kimkakati kwa kutumia PPP ambapo ni lazima aje na mtaji wa
kutosha ambao ataupitishia katika taasisi za kifedha za nchi na kutoa ajira kwa watanzania 1500, lakini
pia watumie malighafi za humuhumu nchini.
Hata hivyo sehemu kubwa bajeti ya mwaka huu imeonesha mapungufu makubwa katika mfumo mzima
wa uwajibikaji wa serikali, katika ukusanyaji wa mapato na hata mgawanyo wake kwa kuangalia
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2014/15. Lakini pia bajeti hii imeelekezwa zaidi kwa sekta binafsi na
wafanyabiashara wakubwa kuliko Watanzania walio wengi ambao ndio wazalishaji wakuu na na walipa
kodi wakubwa; elimu kuwekewa 24% ya bajeti nzima ambayo ni Tshs tril 3.87. hii ni chini ya
makubaliano ya mkataba wa Cairo ambao ni 25% ya bajeti ya nchi Suala kubwa si kiwango cha bajeti
bali ni utekelezaji wa bajeti tajwa kuelekezwa kwenye ujenzi, upatikanaji wa maji shuleni, madawati,
upatikanaji wa chakula mashuleni, umbali, mazingira rafiki kwa mtoto wa kike ambazo zimekuwa
changamoto kwa mtoto wa kike kupata elimu.
Licha ya kuwa serikali imekuwa ikiahidi fedha lukuki kwaajili ya masuala mbalimbali, bado utekelezaji
wa bajeti hizo hauridhishi.Mfano, Mikoa na Halmashauri zimetengewa shilingi bilioni 4,947.8 ikiwa ni
nyongeza ya shilingi bilioni 448.8 ikilinganishwa na Bajeti ya mwaka 2014/15. Lakini hali halisi ya
utekelezai wa ahadi hizo ni wa kutia mashaka na kukatisha tamaa. Mathalani, ripoti ya mkaguzi na
mthibiti wa hesabu za serikali ya 2013/14 inaonesha kuwa utekelezaji hasa katika utoaji wa fedha hizo
ulikuwa si wa kuridhisha.

Ongezeko la Kodi ya pertoli, mafuta ya taa na dizeli.


Tumesikitishwa na kuongezeka kwa kodi kwenye nishati (petrol, dizeli na mafuta ya taa) jambo ambalo
litakalosababisha ongezeko la gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida ambao wengi wao ni
masikini. Hii sio mara ya kwanza kwa serikali kufanya kitendo hiki. Suala hili inaondoa mantiki ya
kupungua kwa kodi ya mshahara na ongezeko la pensheni kwa wastaafu. Kama mnavyojua, mafuta ya taa
ndio tegemeo la nishati kwa wanawake na wanaume maskini na makundi mengine yakiyoko pembezoni.
Na hii itaongeza gharama kwa akina mama wanaojifungua wanaodaiwa kuchangia mafuta katika maeneo
mengi nchini. Mfano katika mikoa ya Morogoro na Shinyanga ambapo wajawazito hununua mafuta ya
taa hadi taa lita tano au kulipa shilingi 10,000 wakati wa kwenda kujifungua. Hii ni kwa mujibu wa
utafiti wa TGNP Mtandao wa mwaka 2015 katika mikoa ya Shinyanga, Morogoro Vijijini, Mbeya Vijini
na Taime, Mara.
Maapitio ya posho na safari za viongozi
Suala la kupitia upya viwango vya posho na safari za viongozi tunaona kama kiini macho kwani wakati
wa bunge la katiba tulimbiwa posho zinapitiwa mwishowe kiwango zikaongezeka. Ni vema kutambua
kua, suala la muhimu si mapitio tu bali ni kupunguza posho hizo lukuki zinazowaneemiesha watu
wachache. Tunaomba umakini katika mapitio hayo kwa kuhakikisha kua viwango vya matumizi hayo
vinapungua badala ya kuongezeka.
Maudhui
Bajeti imeainisha mapato ya shilingi za Kitanzania trilioni 22.4. Kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida
ni shilingi trilioni 16.9 (%) wakati shilingi trilioni 5.6 ni matumizi ya maendeleo sawa na (%).
Tumeshtushwa kuona bajeti ya maendeleo imepungua kwa kiasi cha 0.7 ambayo ni sawa na 12.5% ,
wakati kwa sehemu kubwa ndio tegemeo kwa maendeleo ya Watanzania.
Deni la Taifa
Tumeshangazwa kuona deni la taifa likiongezeka kufikia shilingi za Kitanzania trilioni 35 ukilinganisha
na Trilioni 30.6 katika mwaka wa fedha 2014/15 hivyo kuendelea kuwa kubwa kuliko bajeti ya taifa huku
serikali ikisema kuwa deni hilo ni himilivu. Kwa mwaka ujao wa fedha,mikopo ya nje itakua trilio 25.6
na ndani ni trilioni 9.4. Licha ya kwamba deni hili la taifa linazidi kukua, bado tunashangaa kuona serikali
inasisitiza kuendelea kukopa kwa kigezo cha deni kuwa himilivu na kwamba serikali inakopesheka.
Kutokana na serikali kushindwa kuweka mikakati mizuri ya kiuchumi hususani ya kifedha, thamani ya
shilingi imeendelea kuporomoka na hivo kuathiri deni la taifa.Ni suala la kusikitisha kuona kua kila
mwaka wa fedha thamani ya shilingi imekua ikiporomoka. Wakati huohuo Serikali inashindwa
kusimamia kodi, ulinzi na mgawanyo mzuri wa rasilimali tulizo nazo na inatoa misamaha ya kodi isio na
tija kwa taifa, vilevile upotevu wa fedha kutokana na ufisadi, Mfano ESCROW. Tunadai uwajibikaji wa
serikali katika kusimamia ukusanyaji wa mapato na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato
ambavyo ni endelevu.

Vipaumbele vya Bajeti


Bajeti hii ni ya mwisho katika awamu hii ya nne ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM, mpango wa
maendeleo wa miaka mitano hivyo bajeti hii imeelekezwa katika utekelezaji wa miradi kupitia Malengo
ya Milenia, zaidi katika sekta ambazo zipo katika mpango wa Matokeo makubwa sasa (Maji, Kilimo,
Elimu, utawala bora na miundo mbinu) na Mkukuta II. Serikali imeweka vipaumbele nishati na madini bil
916.7 (5.7%) bila kujumuisha mfuko mkuu wa serikali, kati ya hizo 447.1 zimetengwa kwa ajili ya mradi
wa usambazaji wa umeme vijijini; Miundombinu shingi bil 2,428.8 zimetengwa kwa ajili ya sekta ya
ujenzi na uchukuzi sawa 15.1% ya bajeti yote bila kujumuisha mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya
miundombinu ya usafirishaji, ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja, pia kujenga na kuboresha
bandari; kilimo bil 1,001.4 (6.2%) ya bajeti yote bila kujumuisha bajeti yote ya serikali kwa ajili ya
kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji, ujenzi wa maghala na masoko; elimu bil 3,870.2 (24%) bila
kujumuisha mfuko mkuu wa serikali ili kugharamia ubora wa elimu na mkopo wa wanafunzi; maji bil
573.5 (3.6%) imeelekezwa kuimarisha miundombinu ya maji mijini na vijijini.; Afya imetengewa bil
1,821.1 (11.3) ya bajeti yote ili kuboresha huduma za afya katika ununuzi wa madawa kuzuia magonjwa
ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti ukimwi na malaria. Tunadai rasilimali za
kutosha kutoa huduma bora ya uzazi salama na afya ya jamii.
Katika sekta ya kilimo mkazo umewekwa katika kutoa misamaha ya kodi kwenye pembejeo za kilimo
yakiwemo Matrekta ambayo yataendelea kuagizwa nchini bila ya kulipiwa ushuru. Msamaha huu wa kodi
haujatengeza mazingira ya namna ya kumnufaisha mkulima mdogo nchini na badala yake unanufaisha
wakulima wakubwa na wakodishaji wa matrekta hayo. Jambo hili linaendeleza mfumo wa unyonyaji na
ubepari kwa wakulima wadogo na kupanua wigo wa matabaka kati ya wakulima wadogo na wakubwa na
kuongeza pengo kati ya walionacho na wasiokuwa nacho. Pia mpango huu unaendeleza ulimbikizaji
kiporaji wa ardhi nchini na kuongeza migogoro isiyoisha kati ya wawekezaji na wakulima wadogo, na
wafugaji. Tunadai mgawanyo wa ardhi uendane na mahitaji ya makundi katika maeneo husika
hususani kwa wanawake, vijana na wanaume maskini.
Serikali imeonesha juhudi za makusudi za kutaka kulinda viwanda na bidhaa za ndani kwa kuongeza kodi
kwa bidhaa ambazo zinaagizwa kutoka nje ya nchi. Tunashauri mkakati huo huo ufanywe pia ili
kuwalinda wawekezaji wadogo wanaowekeza kwenye gesi asilia pamoja na mafuta. Hii itasaidia
kuongeza tija kwa wawekezaji wadogo katika uchimbaji pamoja na uvunaji na hatimae itasaidia kuinua
pato la taifa na kupunguza utegemezi wa kibajeti nchini.
Katika hotuba ya bajeti serikali imesema imetoa jumla ya ajira mpya 574,000 ikiwa ni pungufu ya 56,616
ya bajeti ya 2014/15 ambapo serikali ilitoa ajira mpya 630,616 kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha
na idadi ya wahitimu wanaokadiriwa kuwa 1,000,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka
pamoja na wale waliopo tayari. Tunahoji ajira hizi zilizotolewa na serikali kwa mwaka 2014/2015
zinakidhi mahitaji ya soko la ajira? Na Je ajira hizi ni salama na endelevu zinazojali utu, heshima na
staha? Bado tunadai mkakati maalum wa kuendeleza viwanda vya uzalishaji wa malighafi vikubwa na
vidogo vinavyoweza kuongeza ajira kwa waliokuwa wengi vijijini na mijini.

Katika sekta ya elimu serikali imetenga kiasi cha Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya halmashauri 80
kujenga nyumba za walimu. Kiasi kama hiki kilitengwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014 kwa
halmashauri 40 nchini. Tunahoji pesa hizo zilizotumika zilijenga nyumba ngapi na katika halmashauri
zipi na zenye ubora gani? Je upo wapi mkakati wa ujenzi wa mabweni, kuboresha mazingira ya
kufundishia na vifaa vya kujifunzia, na mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu?
Mwisho tumesikitishwa sana kuona Waziri wa Fedha akikiri bungeni kwamba sera zetu za kiuchumi
zinatokana na mashirika makubwa ya kibeberu kama vile IMF kupitia mpango wa Policy Support
Instrument (PSI). Hali hii inathibitisha kwamba mipango mingi iliyopo nchini haitokani na wananchi bali
matakwa ya mashirika makubwa yanayoendeleza ulimbikizaji kiporaji wa rasilimali nchini. Lakini pia
serikali inaendelea kupuuza utaalamu wa wataalamu wa uchumi wa ndani ya nchi.
Madai
Kutokana na uchambuzi ulioainishwa hapo juu tunadai yafuatayo:
1. Kuwepo mfumo shirikishi na endelevu katika kutengeneza na kufatilia utekelezaji wa bajeti ya
taifa na serikali za mitaa kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi, wanawake na wanaume na
makundi yaliyoko pembezoniMisamaha ya kodi katika kilimo ilenge kuwanufaisha wakulima
wadogo wadogo na sio wawekezaji wakubwa.
2. Kukua kwa uchumi wa nchi kuende sanjari na kupunguza umaskini kwa wananchi wote
wanawake na wanaume na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
3. Sekta ya afya ipewe kipaumbele kama zilivyo sekta nyingine katika Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) na kuhakikisha bajeti inafikia 15% ya bajeti ya taifa kama ilivyoagizwa
katika azimio la Abuja.
4. Uwajibikaji zaidi katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali ikiwemo
kuondoa misamaha ya kodi isiyokuwa na tija pamoja na utoaji wa fedha kwa wizara, taasisi na
halmashauri kwa wakati na kiwango stahiki.
Tamko hili limetolewa na:
Sisi wanaharakati wa kikundi kazi cha uchambuzi wa bajeti, wanaharakati kutoka Dar es Salaam, Mbeya,
Morogoro, Shinyanga, Mara na washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS),kwa ushirikiano na
TGNP Mtandao
Imesainiwa na:

Gloria Shechambo,
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
TGNP Mtandao
Tarehe 12 Juni 2015
4

You might also like