You are on page 1of 3

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS
Simu Na: +255 (026) 2963630 Menejimenti ya Utumishi wa Umma
Nukushi: +255 (026) 2963629 na Utawala Bora,
Barua Pepe: ps@utumishi.go.tz Jengo la Taaluma Na. 1,
Tovuti: http://www.utumishi.go.tz Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
Barabara ya Mkalama,
S.L.P. 670,
40404 DODOMA.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAREHE 31 OKTOBA, 2017 KUWA MWISHO WA KUDAI MALIMBIKIZO YA


MISHAHARA KUPITIA FOMU

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuanzia


tarehe 31 Oktoba, 2017 imeelekeza madai ya malimbikizo ya mishahara ya
Watumishi wa Umma kwa kujaza fomu za madai kufikia ukomo. Maafisa
Utumishi wanatakiwa kupokea na kujaza madai hayo kupitia Mfumo wa Taarifa
Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara.

Waziri Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa
Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Tarafa ya Ukonga, kilichofanyika
ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari ya Pugu, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kairuki amesema katika kikao kilichowakutanisha watumishi wa umma


kutoka kata 13 za Ukonga kuwa kumekuwa na adha kubwa ya mlundikano wa
makaratasi ambao umekua ukichelewesha watumishi wa umma kupata haki
zao kwa wakati kwa kupitia hatua mbalimbali, hivyo kuanzia tarehe 31 Oktoba,
2017 kila hatua itafanyika kielektroniki ili kuleta mabadiliko na kuboresha
utendaji kazi.
Nawaagiza waajiri kupitia kwa Maafisa Utumishi kuingiza taarifa za
malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma kwa usahihi ili mfumo
uweze kukokotoa moja kwa moja na malipo kufanyika haraka Mhe. Kairuki
amesema.

Ameongeza kuwa Maafisa Utumishi wawe makini katika kupokea na kujaza


taarifa za watumishi wa umma katika mfumo, pia watumishi nao watoe
ushirikiano wa dhati katika kuweka kumbukumbu za taarifa zao ili wapate haki
yao inavyostahili.

Aidha, Waziri Kairuki amesema Serikali inaendelea kupitia muundo wake upya
ili kupunguza ukubwa, kuunganisha taasisi zinazofanya kazi zinazofanana na
kuleta uwiano sawa wa stahili kwa watumishi wa umma serikalini.

Huko nyuma, tumeshuhudia baadhi ya taasisi za Serikali zikijipangia stahili


mbalimbali pamoja na mishahara, sasa hivi ni lazima kuomba kibali kwa Katibu
Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. Kairuki amesema na kusisitiza lengo ni kuwa na uwiano sawa.

Ameongeza kuwa Serikali ina nia nzuri na inaijali rasimaliwatu yake ambapo
katika zoezi hili tathmini ya kazi inafanyika ili kila kada itendewe haki katika
kupata stahili kulingana na majukumu yake.

Waziri Kairuki katika ziara yake amewataka watumishi kufanya kazi kwa
ushirikiano na kuwasisitiza Maafisa Utumishi kuwasikiliza wateja wao,
wakiwamo watumishi wenzao na kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na
kuwaelemisha kuhusu nyaraka za kiutumishi.
2
Awali akisoma taarifa ya Tarafa ya Ukonga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Ilala, Bw. Msongela Palela amempongeza Mhe, Kairuki kwa
kufanya ziara hizo kwani imewasaidia watumishi wa umma kujua masuala
mengi ya kiutumishi.

Mimi nina mwaka mmoja tangu niingie Halmashauri ya Manipaa ya Ilala lakini
kwa ziara hizi nimejifunza masuala mengi sana ya kiutumishi na hata kwa
watumishi wenzangu nina hakika malalamiko mengi yatapungua, Bw. Palela

Mhe. Kairuki anahitimisha ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama


ambapo leo amekutana na Watumishi wa Umma wa kada zote wa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Tarafa ya Ukonga.

Vikao kazi vilivyofanyika mkoani Dar es salaam, pamoja na ufafanuzi


uliotolewa, zaidi ya hoja 750 zimepokelewa kwa njia ya maandishi ili kufanyiwa
kazi.

Lengo la kukutana na watumishi wa umma ni kusikiliza malalamiko, ushauri na


changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia
kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo
yaliyopangwa na Serikali.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI


OFISI YA RAIS-UTUMISHI
21.07.2017

You might also like