You are on page 1of 4

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI

TAARIFA KWA UMMA

KUHUSU TAARIFA ZA UONGO NA UZUSHI DHIDI YA TUME YA TAIFA YA


UCHAGUZI ZILIZOTOLEWA NA GAZETI LA MWANAHALISI

Katika Maoni ya Mhariri ya Gazeti la MwanaHalisi Toleo Na. 402 la Jumatatu, tarehe 31
Julai 06 Agosti, 2017, yenye kichwa cha habari Kwa hili, NEC imechafuka zaidi.

Maoni ya Mhariri wa gazeti hilo yameonesha kwa mara nyingine na kwa makusudi
kabisa namna ambavyo gazeti hilo siyo tu haliandiki habari sahihi na za kweli kuhusu
NEC bali kutokuwa makini katika uandishi na kutozingatia miiko ya taaluma ya
uandishi wa habari, umakini na weledi wa Mhariri anayeandika maoni yasiyo na
ukweli wowote.

Tume inapenda kukanusha uongo na uzushi huo kwa ufafanuzi ufuatao:

Mosi, majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi yamefafanuliwa vema kwenye Ibara


ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya
Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292,
inaelezea majukumu ya Tume.

Pili, kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 hakijaweka
masharti kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha
kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hali ya migogoro kwenye Vyama vya Siasa
na/au hali (status) ya mashauri yanayohusu migogoro hiyo yaliyofunguliwa
Mahakamani. Kwa mantiki hiyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi si mamlaka ya
kushughulikia masuala ya migogoro ya Vyama vya Siasa na mashauri yaliyoko
Mahakamani yanayohusu migogoro hiyo.

Tatu, baada ya Spika kutekeleza mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 37 (3) cha
Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya kutangaza na kuijulisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu

1
ya uwepo wa nafasi ya wazi ya Kiti cha Ubunge, Tume haina mamlaka Kisheria na
Kikanuni ya kujielekeza katika migogoro ya Vyama vya Siasa na/au mashauri
mbalimbali ya Vyama hivyo yaliyofunguliwa Mahakamani. Tume inao wajibu wa
kujaza nafasi kama hizo kwa kuzingatia masharti yaliyo wazi ya vifungu 37 (3) na 86A
vya Sheria ya Uchaguzi.

Nne, kwa mujibu wa Ibara ya 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya


mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kifungu cha 86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi,
Sura ya 343, Tume hushauriana na Chama cha Siasa husika ili kishauri na kupendekeza
majina ya wanachama wenye sifa za kuteuliwa katika nafasi ya Wabunge wa Viti
Maalum kutoka katika orodha ambayo ilishaletwa na chama husika wakati wa
Uchaguzi Mkuu.

Tano, Tume ilikiandikia barua Chama cha Wananchi - CUF kuhusu uwepo wa nafasi
hizo wazi. kwa kuzingatia masharti ya ibara 78(4) ya kifungu cha 86A(8) cha Sheria ya
Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, CUF walijibu kwa kushauri na kuwasilisha
mapendekezo ya wanaofaa kuteuliwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum kutoka katika
orodha ya majina waliyoiwasilisha wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Sita, kwa mujibu wa ibara 78(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya


mwaka 1977 pamoja na kifungu cha 86A(8) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya
343, majina nane (8) yaliyopendekezwa na CUF kujaza nafasi wazi za Wabunge wa Viti
Maalum ni miongoni mwa majina hamsini na tano (55) yaliyowasilishwa na CUF kwa
barua yenye Kumbukumbu nambari CUF/AK/DSM/KM/003/1A/2015/14 ya tarehe
28/09/2015 ambayo ilisainiwa na Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad.

Saba, Tume katika kujaza nafasi wazi nane (8) za Wabunge Wanawake wa Viti maalum
haikukiuka taratibu zozote za Kikatiba, Kisheria na Kikanuni. Aidha, utaratibu huu
ndiyo uliotumika kujaza nafasi wazi ya viti maalum kwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) tarehe 14 Aprili, 2017 na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
tarehe 04 Mei, 2017.

2
Nane, inasikitisha kuona Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi bila kuwasiliana na Tume
ili kupata taarifa za kweli kuhusu utekelezaji wa majukumu yake, anazingatia taarifa za
uzushi na uongo kutoka CUF na kuandika taarifa zisizo na ukweli na usahihi wowote
kwamba, majina yaliyoteuliwa na Tume kuwa Wabunge wa Viti Maalum hayakutoka
katika orodha iliyowasilishwa na chama husika mwaka 2015.

Tisa, kwa mujibu wa kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa,
Sura ya 292, Tume hutakiwa kuitisha uchaguzi mdogo wa Madiwani mara mbili kwa
kila mwaka ndani ya kalenda ya mwaka. Aidha, uchaguzi mdogo wa kwanza katika
mwaka wa kalenda wa 2017 ulifanyika mwezi Januari, 2017.

Kumi, Aidha, chini ya masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria hiyo, Tume huitisha
Uchaguzi Mdogo wa kujaza nafasi wazi za Madiwani iwapo itakuwa imepokea taarifa
ya uwepo wa nafasi wazi kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa.
Tume inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo wa madiwani wa Kata na kujaza nafasi wazi
za Madiwani wa Viti Maalum baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye
dhamana ya Serikali za Mitaa hivi karibuni.

Kumi na Moja, hivyo, siyo kila wakati inapotokea nafasi wazi ya Udiwani wa Kata
ndani ya kalenda ya mwaka Tume itaitisha uchaguzi mdogo, inategemea na uzingatiaji
wa kifungu cha 13(1)(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292

Kwa kuzingatia maelezo na ufafanuzi huo, madai ya Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi


kwamba, Tume imeshindwa kutangaza ratiba ya uchaguzi mdogo wa nafasi za
madiwani, hazina ukweli wowote, ni uzushi na uongo na zisizo na mashiko.

Hii siyo mara ya kwanza kwa gazeti la MwanaHalisi kuandika habari za uongo na
uzushi dhidi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mfano katika gazeti la MwanaHalisi toleo
Na. 322 la tarehe 18 24 Januari, 2016 liliandika habari za uongo na uzushi kuhusu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Walipotakiwa kuomba radhi, waliomba radhi kwa kwa
barua yenye Kumbukumbu nambari HHPL/ADM/01/02/16 ya tarehe 04 Februari,
2016 iliyosainiwa na Mhariri Mtendaji ambapo aliahidi kusahihisha katika gazeti la
MwanaHalisi la tarehe 08 Februari, 2016 jambo ambalo walifanya.

3
Kwa kuwa, inaonesha dhahiri kwamba, Mhariri aliyeandika tahariri katika gazeti la
MwanaHalisi hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu majukumu ya Tume na hakutaka
kujishughulisha kujielimisha kujua ukweli halisi kabla ya kuandika tahariri yake; na

Kwa kuwa, uandishi wa aina hii siyo tu ni uandishi usiozingatia miiko ya taaluma ya
uandishi wa habari, weledi na umakini; na

Kwa kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetumia fursa hii kutoa elimu na ufafanuzi
sahihi kwa gazeti la MwanaHalisi.

Hivyo basi, inategemewa kwamba, baada ya taarifa hii, Mhariri wa gazeti la


MwanaHalisi kama alivyofanya awali aombe radhi kwa kutoa taarifa za uzushi na
uongo. Aidha, inasisitizawa kabla ya kuandika taarifa kuhusu utekelezaji wa
majukumu ya Tume ni vema akawasiliana na Tume ili kupata taarifa sahihi.

Imetolewa leo tarehe 01 Agosti, 2017 na:

Kailima, R.K
MKURUGENZI WA UCHAGUZI

You might also like