You are on page 1of 8

MASHAIRI

TUWAHESHIMU WAZAZI

Tukiwa ndugu watatu, Modi-Iddi na Waziri

Pamoja na dada zetu, Mima na Hindu mzuri

Na Momo mkubwa wetu, kwa pamoja twakariri

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu

Tukiwa sisi watoto, sote tuwe na adabu

Ukichapwa kwa kikoto, baba akikuadhibu

Usiulete utoto, utakuja pata tabu

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu

Tuwaheshimu wazazi, ndio waliotuzaa

Wazazi wana mapenzi, kwetu sisi manufaa

Mama hupika mchuzi, na sima ikatufaa

Tuwaheshimu wazazi , pamoja na waalimu

Tukitumwa na mzazi, haraka tuitikie

Wewe ukipewa kazi, na baba ifatilie

Hata ya kupanda ngazi, mfanyie mfanyie

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu


Usimtusi mamako, sije ukapata lana

Ugeuke kombamwiko, watu wote kukukana

Mwisho usukumwe huko, jela kwenda ozeana

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu

Mama na baba dhahabu, wanang’ara wavutia

Watupatia vitabu, mashuleni kusomea

Tukiumwa hututibu, hata kama malaria

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu

Pili waalimu wetu, soteni tuwaheshimu

Watufunza kila kitu, hao wetu waalimu

Nidhamu bora ya utu, watufundisha elimu

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu

Bet nane tamatini, tumefika ukingoni

Sote tulio nyumbani, likizo muwe makini

Lakini ela lakini, wazazi waheshimuni

Tuwaheshimu wazazi, pamoja na waalimu

Ushirikiano wa:-

Muhammad Thabit (Baabad)

Iddi Thabit (China boy)

Waziri Thabit (Macho makali)

Al-Miraj Integrated Academy & Tahfidh Quran

Likoni (Likizoni Mwananyamala)


MOYA NA MOYA NI NGAA?

Nakichanganya kiamu, pamoya na kimvita

Thumma nyote mufahamu, ya mashimo na matuta

Ni swali lanidhulumu, ndwele twiba natafuta

Moya na moya ni ngaa?

Wababa Ali Mwanyumba, upesi ninakuita

Utupigie kayamba, vigoma kuvipapata

Imba mwanakwetu imba, tatuwa huno utata

Moya na moya ni ngaa?

Tupa ya soda ngaramba, mrija kuvutavuta

Na mzizi kuuchimba, ngama mihogo kupata

Ni fumbo nimelifumba, gogo naligotagota

Moya na moya ni ngaa?

Mohammedi wa Shabani, mpambuzi nakuita

Matishali mwanapwani, ng’ara mithili ya nyota

Noti usambe ni peni, chambua jibu kuleta

Moya na moya ni ngaa?

Habiba Chea ingia, kirumbizi kusakata

Mkubwa wa hizo pia, Maliki Dhudhu pepeta

Mwapopho nakuchochea, nishazibwaga karata

Moya na moya ni ngaa?


Ndhoo mwanangu sikia, Momo wa Thabiti leta

Jawabu la kuridhia, mtihani kuupata

Beti zote kutimia, ndoo siriye ni kata

Moya na moya ni ngaa?

Nduu yangu Babu lao, Chatu Barro nakufata

Shee Ngare teza bao, na Mbogholi wa Taveta

‘Richi Begger ‘ mwanakwao, goma nimeshalikita

Moya na moya ni ngaa?

Mwanakwechu huko Amu, Mamswabu shika mita

Mbwajumwali wafahamu, wapate wote kufata

Hindi Mokowe sehemu, kwa labania kashata

Moya na moya ni ngaa?

Sambi mangi natulia, natuliza tarumbeta

Jawabu natazamia, Pambazuko kulipata

Na swababu kutimia. Si bure kubwatabwata!

Moya na moya ni ngaa?

Utunzi wa:

‘Joka Kuu’

Mzawa Mvita

Majengo King’orani

Mombasa
UREMBO NI ASILIA

Kalamu ninaishika, nitowe langu tamko

Yanishangaza mashaka, wanawake walioko

Wakana Uafrika, weusi kwao ni mwiko

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Wewe dada umweusi, kwanini hauutaki?

Ni rangi yako nyeusi, inapaswa ujinaki

Uzungu wapiga pasi, weusi wako hutaki

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Ni Mola alokuumba, alompa yule kiti

Kumbi wewe hukuomba, Mola kakupa uketi

Wazungu pia huimba, kweli ‘Black is beuty!’

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Kutwa wavaa mawigi, huzitaki nyele zako

Wanuka kama huogi, uvundo mawigi yako

Nyele asili hufugi, makofia vibandiko!

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Wabadili ngozi yako, eti wataka weupe

Wachekesha uso wako, mabatobato meupe

Tena makwapa na huko, umweusi humweupe!


Urembo ni asilia, si wigi si mikorogo

Kama mwanga mkorogo, weupe wa kuzidia

Wajiita ndogo ndogo, madawa unajitia

Mwisho chatoka kisogo, watu wakuchekelea!

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Wengine hujipa tabu, sindano kushindilia

Afutuke taarabu. Na matiti kuzidia

Mwisho hutisha kurabu, sura kama ya ngamia!

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Mawigi ya kila rangi, samawati na manjano

Nyekundu na hudhurungi, sura kama konokono

Wabomowa hawajengi, watisha waume mno!

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo

Thamini yako asili, alokuumba Jalali

Ni chako kipilipili, kitunze usibadili

Chakwako ni afadhali, cha mwenzako idhilali

Urembo ni asilia. Si wigi si mkorogo

Kaditamati watama , nilonena samahani

Kinadada kinamama, ushangingi tuacheni

Kemikali kujichoma, tawadhuru si utani

Urembo ni asilia, si wigi si mkorogo


Utunzi wa:-

Momo Thabit ‘Mamaa”

Shule ya upili ya Wasichana ya Karima

Kidato cha 4 Lagoon

Nyandarua

(Likizoni Bomani-Likoni)

Mombasa

PAMBAZUKO JUU JUU!

Nalisifu gazeti, Pambazuko nalisifu

Gazeti hili smati, la mapana na marefu

Linapendwa na umati, watu wengi walisifu

Pamabazuko juu juu!

Tulisinywa masikini, na kigazeti fulani

Hawajui hayawani, Kiswahili chenye shani

Mara shengi mara nini, watembea hawaoni

Pambazuko juu juu!

Pambazuko limezuka, na makala mbali mbali

Kisiasa wakawaka, ujibiwe na maswali

Mengi ya kuelimika, fasihi ya kisukuli

Pambazuko juu juu!


Kuna ule ukrasa, wa michezo tunapenda

Habari moto za sasa, za riadha na kandanda

Lugha poa ya kisasa, utacheka utapenda

Pambazuko juu juu

Na mwenda tezi na omo , tamati huwa ngamani

Nami sasa hapa simo, nimefika kituoni

Tusomeni yaliomo, gazeti pambazukoni

Pambazuko juu juu!

Utunzi wa:

Hindu Thabit

Waa Boarding Primary School

Waa-Kwale

You might also like